Home Kitaifa WAZAZI: WATOTO WAMEKUWA MABALOZI WA VIPIMO KATIKA JAMII

WAZAZI: WATOTO WAMEKUWA MABALOZI WA VIPIMO KATIKA JAMII

 

Na Alex Sonna, Dodoma

WAZAZI jijini Dodoma wamesema elimu ya vipimo inayotolewa kupitia Klabu za Vipimo katika shule za msingi imeanza kuleta mabadiliko ndani ya familia, baada ya watoto waliopatiwa mafunzo na Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kuanza kuwafundisha wazazi wao namna ya kutambua vipimo sahihi na kujilinda dhidi ya upunjaji katika manunuzi.

Wazazi wameyasema hayo  Septemba 18,2026  wakati wa mahafari ya wanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Mtemi Mazengo jijini Dodoma ambapo  wanafunzi wa klabu ya vipimo walikuwa wakitoa elimu ya vipimo kwa wazazi na watu wengine mbalimbali waliohudhuria akiwemo Mgeni Rasmi.

Mzazi wa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mtemi Mazengo, Bertha Paulo Chipaga, amesema mtoto wake, Gloria Elisha Enock, amekuwa akimsaidia kuelewa matumizi sahihi ya mizani ya chakula, mita ya maji na vipimo vingine, jambo ambalo limempa uelewa na kujiamini zaidi kama mlaji.

Bi.Chipaga amesema awali hakuwa na uelewa mpana kuhusu namna ya kutambua kama kipimo kinachotumika katika biashara ni sahihi, lakini tangu mtoto wake ajiunge na Klabu ya Vipimo amekuwa akipata elimu hiyo nyumbani na sasa anaelewa umuhimu wa kuhakikisha bidhaa anayonunua inalingana na kiasi cha fedha anacholipa.

“Hatua hiyo inaonesha kuwa elimu inayotolewa kwa watoto haiishii shuleni, bali inasambaa hadi kwenye familia na jamii, hivyo akawataka wazazi wengine kutumia fursa hiyo kuwaelimisha watoto wao kuhusu haki za mlaji na matumizi sahihi ya vipimo.”amesema Bi.Chipaga

Akizungumza kuhusu umuhimu wa kuwaandaa watoto na elimu hiyo, mkazi wa Makao Mapya jijini Dodoma, Peter Daudi Mponzi, amesema mafunzo ya vipimo kwa wanafunzi ni uwekezaji muhimu kwa jamii kwa sababu yanawajengea uwezo wa kutambua mizani na vipimo visivyo sahihi wanapokuwa katika mazingira ya biashara.

Amesema mtoto anayeelewa vipimo anaweza kwenda dukani na kuangalia kama mzani unaotumika umehakikiwa, hivyo kupunguza uwezekano wa yeye au familia yake kupunjwa na wakati huo huo kueneza elimu hiyo kwa watu wengine.

Mponzi amesema kuanzia elimu hiyo katika umri mdogo kunaweza kujenga kizazi chenye uelewa mpana wa masuala ya vipimo na haki za walaji, kwa kuwa watoto wanakuwa na nafasi ya kutumia maarifa hayo katika maisha yao ya kila siku.

 “Watoto wanapotoka shuleni na kwenda majumbani, dukani na katika maeneo mengine ya jamii, wanakuwa sehemu ya mnyororo wa elimu unaoweza kuwafikia wazazi, ndugu na wananchi wengine, hivyo kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi.”amesema

Mwanafunzi wa Klabu ya Vipimo katika Shule ya Msingi Mtemi Mazengo, Gloria Elisha Enock, amesema WMA imewajengea uwezo wa kuelewa maana na umuhimu wa vipimo pamoja na jukumu la Wakala la kumlinda mlaji.

Amesema wamefundishwa kuwa WMA huhakiki vipimo mbalimbali, ikiwemo mizani, mita za maji na umeme, pamoja na bidhaa zilizofungashwa, huku mlaji akitakiwa kuangalia alama ya WMA kwenye mizani ili kuhakikisha kipimo  hicho kimehakikiwa na kinafanya kazi kwa usahihi.

Kwa upande wake, mwanafunzi mwenzake, Venosa Michael Simba, amesema elimu hiyo imemsaidia kubadilika kutoka kuwa mtoto anayekwenda dukani bila kuzingatia usahihi wa vipimo hadi kuwa mfuatiliaji na mtoa elimu kwa jamii.

Amesema baada ya kupata mafunzo hayo aligundua hata nyumbani kwao kuwa mita ya maji ilikuwa haijahakikiwa na akaweza kutoa elimu kwa watu waliokuwa hawajui umuhimu wa kuhakiki vipimo.

 “kabla ya kupata elimu hiyo alikuwa akienda dukani bila kuangalia chochote, lakini sasa anaelewa kuwa mlaji ana wajibu wa kuhakikisha anapata kiasi sahihi cha bidhaa anayolipia.”amesema

Kwa ujumla, Klabu za Vipimo za WMA zimeanza kuwa darasa la vitendo la kuwaandaa watoto kuwa mabalozi wa ulinzi wa mlaji, huku elimu hiyo ikitoka shuleni na kuingia moja kwa moja katika familia na jamii.

Mpango huo unaongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya vipimo sahihi, unasaidia kujenga utamaduni wa kuhoji na kuthibitisha vipimo vinavyotumika katika biashara na, kwa muda mrefu, unaweka msingi wa kizazi kinachothamini uadilifu, usawa na uwazi katika shughuli za kiuchumi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!