
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Shirika la African Leadership Initiatives for Impact (ALII), kwa kushirikiana na HakiElimu na kwa uwezeshaji wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania, Norwegian Church Aid na UTT AMIS, limezindua awamu ya pili ya Programu ya Tanzania NextGen Leaders Fellowship (TNLF Cohort 2), inayolenga kuwaandaa vijana kuwa viongozi wenye maono, maadili na uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa.
Uzinduzi wa programu hiyo umefanyika leo katika Ukumbi wa Maktaba Mpya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ukihudhuriwa na vijana 100 waliochaguliwa kushiriki katika kundi hilo, pamoja na viongozi, wataalamu, wadau wa maendeleo na wawakilishi wa taasisi mbalimbali.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Dkt. Redmond Mapana, amesema uwekezaji katika kuwajengea vijana uwezo wa uongozi tangu mapema ni muhimu katika kuhakikisha Tanzania inapata kizazi cha viongozi wenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kukabiliana na changamoto za maendeleo.
Amesema programu hiyo inatoa fursa kwa vijana kujifunza misingi ya uongozi, uzalendo, maadili na uwajibikaji, akiwataka kutumia maarifa watakayoyapata katika mafunzo hayo kujijengea uwezo na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Dkt. Mapana amesema ushiriki wa vijana katika masuala ya maendeleo ni muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Mary Ndaro, amesema programu hiyo imewakutanisha zaidi ya vijana 100 kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwapatia maarifa katika nyanja mbalimbali, hususan uongozi.
Ndaro amesema mafunzo hayo yanawawezesha vijana kubadilishana uzoefu, kujifunza kutoka kwa wataalamu na kujenga uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika jamii.
Amesema uwekezaji katika kuwaandaa vijana kuwa viongozi bora ni hatua muhimu katika kujenga kizazi chenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na taifa.
Kwa mujibu wa waandaaji, programu ya TNLF inalenga kuwajengea vijana ujuzi na mtazamo wa uongozi utakaowawezesha kuwa sehemu ya mabadiliko chanya katika jamii, huku wakitumia uwezo wao katika kuchangia maendeleo ya Tanzania.







