Home Kitaifa PWANI YETU YAWAPA KICHEKO WAKAZI WA MWAMBANI, TANGA

PWANI YETU YAWAPA KICHEKO WAKAZI WA MWAMBANI, TANGA

Na Boniface Gideon, TANGA

Wakazi wa Kata ya Tanga Sisi, mtaa wa Mwambani Jijini Tanga, wamepatiwa shilingi milioni 10.5. Fedha hizo zinalenga kuwaongezea mitaji wavuvi na wafanyabiashara, hususan wa samaki, ili wapunguze utegemezi wa shughuli za kiuchumi baharini ambazo husababisha uhalifu, ikiwemo ukataji wa mikoko na uvuvi haramu pamoja na uchafuzi wa fukwe za bahari.

Fedha hizo zimekabidhiwa jana na Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania kupitia Mradi wa Pwani Yetu unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), Wizara ya Shirikisho ya Ujerumani ya Hatua za Tabianchi, Hifadhi ya Mazingira, Usalama wa Nyuklia na Ulinzi wa Mtumiaji (BMUKN), pamoja na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU).

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya fedha hizo kati ya wananchi na viongozi wa mashirika hayo, Mratibu wa Shirika hilo Mkoa wa Tanga, Ahmed Salim, alisema fedha hizo zimetolewa kwa vikundi 5 vyenye wanachama 150, kati yao wanaume 40 na wanawake 110.

Fedha hizi tunazitoa kwa wanachama 150 ambao tumewafundisha na kuwapatia mafunzo ya elimu ya fedha, utunzaji wa mazingira hususani bahari na rasilimali zake. Lengo la kutoa fedha hizi ni kuwasaidia wanachama kupunguza shughuli za kiuchumi baharini kwa kuongeza mitaji ya biashara zao ili kupunguza utegemezi wa bahari,” aliongeza Ahmed.

Ahmed alisema fedha hazirejeshwi kwa shirika hilo bali wanachama waliokabidhiwa wanajiwekea utaratibu wa kukopeshana bila riba.

Sisi tunakabidhi fedha kwa wanachama, hivyo wao wanajiwekea utaratibu wa kukopeshana bila riba ili fedha hizi ziwepo kwenye mzunguko wa kila siku. Tunaamini fedha hizi zitawasaidia wanachama hawa, ikizingatiwa kuwa wengi wao ni wanachama wa BMU na maisha yao yanategemea bahari, hivyo tuna imani kubwa na wanachama hawa kuwa watakuwa mabalozi wazuri wa mazingira.

Tunaamini kuwa kupitia fedha hizi, mtaongeza vipato vyenu na mtakuwa mabalozi wazuri wa utunzaji wa mazingira, hususani upandaji wa mikoko, utunzaji wa fukwe na uvuvi salama. Pia tunaamini kuwa mtakuwa wasimamizi wa rasilimali za bahari na kuongeza vipato vyenu,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Tongoni, Bunu Omar, alilishukuru shirika hilo kwa kutoa fedha ambazo zimelenga kuwainua kiuchumi wakazi wa kata hiyo wengi wao wanategemea bahari kuendesha maisha yao.

Tunashukuru sana kwa kupata fedha hizi. Hali ya uhalifu baharini ni mbaya, kwa hiyo kupitia fedha hizi kila mmoja wetu atakuwa na kazi nyingine nje ya bahari. Hii itatusaidia kuongeza vipato vyetu, lakini pia kwa sisi tunaofanya doria baharini tutakuwa wengi zaidi, kwa kuwa kila mmoja wetu amepata elimu ya mazingira pamoja na faida zake,” alisisitiza Kombo.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!