Home Kitaifa Dkt. Samia Aanika Mipango Mikubwa ya Maendeleo Akiendelea na Kampeni Mkoani Pwani...

Dkt. Samia Aanika Mipango Mikubwa ya Maendeleo Akiendelea na Kampeni Mkoani Pwani Leo

Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumapili Septemba 28, 2025, anatarajiwa kuendelea na kampeni zake Mkoani Pwani kwa ajili ya kunadi Ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030 pamoja na kuomba kura kwa wananchi wa mkoa huo.

Dkt. Samia, ambaye tayari ametembelea mikoa ya kusini ikiwemo Mtwara, Lindi na Ruvuma akinadi sera na kuomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, leo ataendelea na mikutano ya kampeni kuanzia Wilaya ya Kibaha, kisha Chalinze, na baadaye Msata. Katika maeneo hayo atafanya mikutano mikubwa ya hadhara kabla ya kuelekea kwenye mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwemo Tanga na Arusha.

Akiwa Mtwara Mjini katika mkutano wa kuhitimisha kampeni zake mkoani humo, Dkt. Samia aliahidi kuimarisha sekta ya kilimo hususan zao la korosho, kwa kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo na huduma za ugani ili kuiwezesha Tanzania kuendelea kuwa mzalishaji mkubwa wa zao hilo. Aidha, aliahidi kuunganisha Mkoa wa Mtwara na njia zote za usafirishaji, ikiwemo ujenzi wa reli kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay, ili kurahisisha biashara na kuongeza ushirikiano na nchi jirani za Msumbiji na Malawi.

Kadhalika, Dkt. Samia aliahidi kuendelea kutafuta masoko ya uhakika ya mazao ya kilimo kama korosho, mbaazi na ufuta; kukamilisha mradi wa umeme utakaoziunganisha Mtwara na Lindi kwenye gridi ya Taifa; pamoja na ujenzi wa vituo vya kupooza umeme ili kuhakikisha mikoa hiyo inaondokana na tatizo la umeme usio wa uhakika. Vilevile, alisisitiza dhamira ya serikali kuwekeza zaidi kwenye teknolojia katika sekta mbalimbali na kuchukua hatua madhubuti za kulinda mila na desturi za Kitanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!