Na. Shomari Binda
WIZARA ya Maliasili na Utalii imempongeza mbunge wa viti maalum mkoa wa Mara, Agness Marwakwa kutetea na kufatilia maslahi ya wananchi wa mkoa wa Mara.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Marryprisca Mahundi wakati akijibu swali la mbunge huyo aliyetaka kujua malipo ya wananchi wa vijiji vya Kata ya Nyatwari wilayani Bunda.
Katika swali lake la msingi mbunge huyo alitaka kujua namna serikali ilivyojipanga kuwatafutia maeneo wananchi waliopisha uthamini kwenye maeneo yao.
Akijibu swali la mbunge huyo kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Naibu Waziri huyo amesema uthamini kwenye maeneo hayo ambayo serikali imeyatwaa upo kwenye hatua za mwisho na mara baada ya kukamilika wahusika watalipwa haki zao.
Amesema wahusika pamoja na malipo mengine watalipwa thamani ya ardhi, mazao, fedha za kujikimu na usumbufu kwa mujibu wa sheria.
Naibu Waziri huyo amesema serikali kupitia halmashauri ya mji wa Bunda imetenga na kupima eneo la viwanja 350 ambavyo watapewa wananchi waliopisha maeneo.
“Nichukue nafasi hii kumpongeza mheshimiwa Agness Marwa, mbunge wa viti maalum mkoa wa Mara kwa kuwatetea na kuwasemea wananchi wa mkoa huo”
“Serikali inayatwaa maeneo hayo kwa maslahi ya Taifa na mara baada ya tathmini wananchi husika watalipwa kwa mujibu wa sheria” ,amesema Naibu Waziri huyo.
Katika maswali yake ya nyongeza mbunge huyo alitaka kujua kiwango cha kuongezewa fedha wananchi kutoka milioni 2 hadi 6 na maeneo ya ufugaji na uvuvi kwa wananchi.








