
Wizara ya Fedha imetoa rai kwa wadau kutoa maoni yatakayowezesha kuboresha Rasimu ya Mwongozo wa Usimamizi wa Mali za Umma wa mwaka 2025 utakaosaidia kusimamia mali zilizo kwenye Taasisi za Umma kwa tija na ufanisi zaidi ili kuimarisha na kuboresha huduma zinazotolewa na Serikali kupitia mali hizo.

Rai hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Chotto Sendo, wakati akifungua kikao kazi cha kukusanya maoni ya wadau kutoka taasisi 25 za Umma zinazowakilisha Mkoa wa Dodoma, Wasimamizi wa Mali wa Mikoa kutoka mikoa saba (7), Wasimamizi wa Mali za Serikali kutoka Ofisi ya Makao Makuu na Mkoa wa Dodoma, kuhusu Rasimu ya Mwongozo wa Usimamizi wa Mali za Umma wa mwaka 2025, kilichofanyika katika ukumbi wa Kilimanjaro, Treasury Square, Jijini Dodoma.

Bw. Sendo alisema, Rasimu ya Mwongozo wa Usimamizi wa Mali za Umma wa mwaka 2025, ambao wadau wanatarajiwa kutoa maoni ya kuuboresha inatokana na fursa mbalimbali zilizojitokeza katika usimamizi wa mali za umma katika kipindi cha utekelezaji wa Mwongozo wa Usimamizi wa Mali za Umma wa mwaka 2019.
‘‘Nawaasa kila mmoja wetu ahakikishe anashiriki kikamilifu kwa kutambua kuwa Mwongozo huu ni nyenzo muhimu itakayowezesha usimamizi bora wa Mali za Umma katika Taifa letu ikizingatiwa kuwa kwenye Rasimu hii ya Mwongozo wa Usimamizi wa Mali za Umma, masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa mali yameelezwa ikiwemo majukumu na wajibu wa usimamizi wa Mali za Umma kwa Watendaji, Wakuu wa vitengo na Wakuu wa Idara mbalimbali katika Taasisi za Umma,’’alisema Bw. Sendo.
Aliongeza kuwa rasimu hiyo pia imejumuisha usimamizi wa mali chini ya ushirikiano wa umma na binafsi (PPP-Projects), Upatikanaji wa mali, matumizi ya mali, usimamizi wa mali za miradi, kushughulikia ajali na potevu za mali za Umma, Ufutaji na uondoshaji wa mali chakavu pamoja usajili wa vyombo vya moto.
Alisema kuwa mwongozo huo utakapokamilika na kusainiwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali (PMG) utaanza kutumika pamoja na Kanuni za Usimamizi wa Mali za Umma za mwaka 2024 hivyo kuwataka kujadili kwa uwazi ili kujenga uelewa wa pamoja katika suala la usimamizi wa mali za umma na kuhakikisha utendaji bora ,uwajibikaji wa kifedha na utoaji wa huduma bora.
Bw. Sendo aliwasisitiza wadau hao kuhakikisha kuwa Mwongozo huo utakapokamilika unatumika kikamilifu ili kutumia fursa zilizopo na zitakazojitokeza baadaye katika usimamizi wa mali za umma.
Aidha, Bw. Sendo alieleza kuwa Wizara ya Fedha imepewa jukumu la usimamizi wa Mali za Umma kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma, Sura 348 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2024 ambapo hutekeleza jukumu hilo kupitia Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali (GAMD) yenye ofisi zake za mikoa ambazo zinahudumia taasisi zote za Umma zilizopo katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.
‘‘Kutokana na wingi wa rasilimali mali tulizonazo inatupa picha ya wingi wa gharama ambazo Serikali imekuwa ikizitumia katika upatikanaji na utunzaji wa mali hizo, hii inatupa kila sababu ya kuwa na mikakati madhubuti ya kuzisimamia mali hizo ili ziweze kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa na kuiwezesha Serikali kupata manufaa ya uwekezaji uliokusudiwa kwa kipindi kirefu’’, alifafanua Bw. Sendo.
Aliongeza kuwa Wizara ya Fedha ikiwa na dhamana ya Usimamizi wa Mali za Umma nchini imefanya jitihada mbalimbali katika kuongeza ufanisi wa Usimamizi wa Mali za Umma nchini ikiwemo kusimika na kuwezesha matumizi ya mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mali za Serikali “Government Assets Management Information Systems – (GAMIS) ambao unatumika kutunza na kuchakata taarifa za mali za Taasisi zote za Umma nchini.
Mmoja wa washiriki wa kikao kazi hicho Msimamizi wa Mali za Serikali Mkoa wa Tabora, Bi. Karerema Kwareh, alieleza kuwa kikao hicho kitawawezesha wadau kujadiliana kwa kina kuhusu mwongozo huo na kujenga uelewa wa pamoja utakaowezesha kuwa na mwongozo sahihi katika usimamizi wa mali za umma.
Kikao kazi hicho cha siku moja kiliandaliwa na Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Usimamizi wa Mali za Umma kimekutanisha wadau kutoka taasisi 25 za Umma zinazowakilisha Mkoa wa Dodoma, pamoja na Wasimamizi wa Mali wa Mikoa kutoka mikoa saba (7), sambamba na Wasimamizi wa Mali kutoka Ofisi ya Makao Makuu na Mkoa wa Dodoma.








