Home Kitaifa WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA AHIMIZA UZALISHAJI WA BIDHAA ZA NDANI

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA AHIMIZA UZALISHAJI WA BIDHAA ZA NDANI

By Magreth Zakaria

Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ametoa wito kwa wazalishaji na wawekezaji kuendelea kuimarisha uzalishaji wa bidhaa nchini ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wa taifa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Desemba 18, 2025, wakati wa kikao na waandishi wa habari pamoja na watumishi wa umma, Waziri Kapinga amesema uzalishaji wa ndani ni nguzo muhimu katika kuimarisha uchumi wa taifa na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Ameeleza kuwa sekta ya viwanda inaendelea kuimarika, huku baadhi ya viwanda vya saruji, tiles (marumaru) na mabati vikiongeza kiwango cha uzalishaji na kusambaza bidhaa kwa wingi sokoni.

Hata hivyo, Waziri Kapinga amekiri kuwapo kwa changamoto zinazokabili baadhi ya viwanda, zikiwemo uhaba wa nishati, gharama za malighafi na changamoto katika usambazaji wa bidhaa. Amesema serikali inaendelea kuweka sera na mikakati itakayopunguza vikwazo hivyo na kurahisisha shughuli za biashara.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kushirikiana na wajasiriamali wadogo, akibainisha kuwa uwekezaji katika uzalishaji wa ndani utatoa fursa zaidi za ajira kwa vijana na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

Kwa upande mwingine, mamlaka husika zimetakiwa kushirikiana kwa karibu na wajasiriamali ili kuhakikisha bidhaa zinazalishwa kwa kiwango kikubwa huku zikizingatia viwango vya ubora na usalama wa watumiaji, hatua itakayosaidia kuongeza pato la taifa na kukuza biashara za ndani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!