Home Kitaifa WAZIRI MKENDA ATAKA ONGEZEKO LA WANAWAKE NA WASICHANA KATIKA TAALUMA ZA SAYANSI

WAZIRI MKENDA ATAKA ONGEZEKO LA WANAWAKE NA WASICHANA KATIKA TAALUMA ZA SAYANSI

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof. Adolf Mkenda,akizungumza wakati wa  hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi yaliyofanyika leo  Februari 11, 2026 jijini Dodoma.

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof. Adolf Mkenda,akizungumza wakati wa  hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi yaliyofanyika leo  Februari 11, 2026 jijini Dodoma.

NAIBU  Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi,akizungumza wakati wa  hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi yaliyofanyika leo  Februari 11, 2026 jijini Dodoma.

WANAFUNZI Wakimsikiliza Waziri  wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof. Adolf Mkenda (hayupo pichani) wakati wa  hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi yaliyofanyika leo  Februari 11, 2026 jijini Dodoma.

SEHEMU ya washiriki  Wakimsikiliza Waziri  wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof. Adolf Mkenda (hayupo pichani) wakati wa  hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi yaliyofanyika leo  Februari 11, 2026 jijini Dodoma.

Waziri  wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof. Adolf Mkenda,akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi  wakati wa  hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi yaliyofanyika leo  Februari 11, 2026 jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof. Adolf Mkenda, amesema takwimu zinaonesha kuwa wanawake wanasayansi duniani ni asilimia 36 pekee, hali inayoashiria kuwepo kwa pengo kubwa la kijinsia katika taaluma za sayansi.

Akizungumza leo Februari 11, 2026 jijini Dodoma katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi, Prof. Mkenda amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi, asilimia 51 ya Watanzania ni wanawake, jambo linaloonesha kuwa bado kuna fursa kubwa ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya sayansi nchini.

“Hali hiyo inaonesha kuwa bado kuna haja ya kuongeza kwa kasi idadi ya wanawake katika taaluma za sayansi ili kuendana na mabadiliko ya kidunia,” amesema Prof.Mkenda

Amesisitiza kuwa ushiriki mkubwa wa wanawake katika sayansi utachangia kukuza ubunifu, tafiti na teknolojia zitakazosaidia taifa kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo.

Aidha  Prof. Mkenda, amesema umefika wakati kwa wanawake na wasichana  kujitokeza kwa wingi kuwekeza na kushiriki kikamilifu katika masuala ya sayansi ili kupanua wigo wa maarifa na kuleta mabadiliko ya kimaendeleo nchini.

Amesisitiza  umuhimu wa kuwahamasisha wasichana kuanzia ngazi ya elimu ya msingi na sekondari kupenda masomo ya sayansi ili kujenga kizazi chenye uwezo wa kushindana kimataifa.

Akizungumzia umuhimu wa sayansi katika sekta ya afya, Prof. Mkenda amesema sayansi imekuwa chachu ya kupunguza vifo vya watoto na kuimarisha maisha ya wananchi kwa ujumla kupitia maboresho ya huduma za tiba, kinga na tafiti za kitabibu.

Aidha, ametoa wito kwa wadau wa elimu na jamii kwa ujumla kuendelea kuwahamasisha wasichana kusoma masomo ya sayansi ili kuongeza idadi ya wataalamu wanawake na kuleta uwiano unaohitajika katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema Tanzania imepiga hatua katika kuimarisha malezi bora kwa mtoto wa kike, jambo linalotoa fursa kwa wasichana wengi zaidi kusoma masomo ya sayansi na hivyo kuepuka ushindani mkubwa katika soko la ajira.

Amesema jitihada hizo zimeongeza mwamko kwa wanawake na wasichana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, sekta ambazo ni mhimili wa maendeleo ya taifa.

Aidha, amesisitiza kuwa usawa wa kijinsia katika elimu ni msingi muhimu wa kufikia maendeleo endelevu, akitoa wito kwa wazazi, walimu na jamii kwa ujumla kuendelea kuwaunga mkono wasichana katika safari yao ya kielimu, hususan katika masomo ya sayansi na teknolojia.

Naye Mwakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Mabula Magangila, amesema sayansi ni suluhisho la changamoto za kidunia na kwamba mtoto wa kike akihamasishwa zaidi anaweza kufanya vizuri hata kuliko mtoto wa kiume.

Ameongeza kuwa wanawake wana utulivu mkubwa wa akili unaoweza kuwasaidia kufanya vizuri katika taaluma za sayansi. Aidha, amesema Serikali imeboresha mazingira ya elimu ya sayansi na kwamba Bunge litaendelea kutunga sera bora zitakazomuwezesha mtoto wa kike kupata haki sawa ya elimu, hususan katika masomo ya sayansi.

Amesisitiza kuwa umefika wakati wa kuhakikisha mtoto wa kike anapewa haki na fursa sawa na mtoto wa kiume katika elimu, hasa katika mazingira ya sayansi na teknolojia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!