
Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa wametakiwa kuweka mifumo rafiki itakayowawezesha wananchi kuwasilisha kero zao kwa urahisi na kupata suluhu ya kudumu.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Jafar Seif, wakati akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Mwanza waliofika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Said Mtanda, kuwasilisha kero zao kupitia utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi unaofanyika kila siku ya Jumanne.

Naibu Waziri alisema kuwa wananchi wanapaswa kusikilizwa na kupewa majibu ya kero na changamoto zao, hasa zile zinazohitaji msaada wa kitaalamu, kisheria na maamuzi ya kiutawala, akisema hatua hiyo itapunguza malalamiko na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wananchi.
“Uwajibikaji ni pamoja na kuwasikiliza wananchi; nampongeza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na kusisitiza viongozi wengine waige mfano huu, wawatumikishe wataalamu waliopo kuwasikiliza wananchi na watende haki ili kuleta tabasamu kwa wananchi wetu wanaohitaji huduma,” alisema Dkt. Seif.

Aliongeza kuwa kipimo cha utendaji kwa wasaidizi wa Rais ni namna wanavyoshughulikia na kutatua kero za wananchi, akisisitiza kuwa changamoto zinazoweza kumalizika katika ngazi za chini zinapaswa kumalizika huko, na pale zinaposhindikana ndiko ziwasilishwe wizarani.
Kwa sasa, Dkt. Seif yuko katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza kukagua utekelezaji wa miradi ya afya inayotekelezwa na Serikali, pamoja na kufuatilia utoaji wa huduma za afya katika vituo mbalimbali mkoani humo.








