Home Kitaifa WATANZANIA WANAOSAFIRI KWENDA MAREKANI WATAKIWA KUZINGATIA MASHARTI YA VIZA ZAO

WATANZANIA WANAOSAFIRI KWENDA MAREKANI WATAKIWA KUZINGATIA MASHARTI YA VIZA ZAO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewataka Watanzania wanaosafiri kwenda Marekani kuzingatia masharti ya viza walizopewa, ikieleza kuwa ukiukwaji wa masharti hayo umechangia Tanzania kuwekwa katika kundi la nchi zenye vikwazo vya sehemu vya kuingia nchini Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliyotolewa Desemba 17, 2025, Serikali ya Marekani ilitangaza kuiweka Tanzania katika orodha hiyo kupitia Rais wake Donald Trump mnamo Desemba 16, 2025, huku ikibainisha kuwa vikwazo hivyo si vya jumla na Watanzania wanaokidhi masharti ya uhamiaji wataendelea kuruhusiwa kuingia nchini humo.

Imeelezwa kuwa uamuzi huo umetokana na idadi kubwa ya Watanzania wanaosafiri kwenda Marekani kushindwa kuzingatia masharti ya viza zao, hususan kwa kukaa zaidi ya muda ulioruhusiwa kisheria, hali iliyooneshwa katika Overstay Report ya Serikali ya Marekani.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa asilimia 8.3 ya wenye viza za B-1/B-2 na asilimia 13.97 ya wenye viza za F, M na J walikaa nchini Marekani zaidi ya muda ulioruhusiwa, viwango vilivyo juu ya vinavyokubalika chini ya sera za uhamiaji za Marekani.

Kutokana na viwango hivyo, Tanzania imejumuishwa katika orodha ya nchi zilizo chini ya vikwazo vya sehemu pamoja na Angola, Benin, Côte d’Ivoire, Gabon, Gambia, Malawi, Mauritania, Nigeria, Senegal, Zambia na Zimbabwe.

Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa inaendelea na mazungumzo ya kidiplomasia na Serikali ya Marekani kutafuta suluhisho la haraka na la kudumu, huku ikiwasihi Watanzania wanaosafiri kwenda nchini humo kuzingatia masharti ya viza zao, ikiwemo kuondoka mara tu muda wa viza unapokamilika, ili kulinda hadhi ya nchi na kusaidia kuondolewa kwa vikwazo hivyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!