WAKAAZI wa Kata ya Kirumba Manispaa ya Ilemela wamepongeza serikali ya awamu ya sita kwa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita moja kwa kiwango cha lami katika Mtaa wa Magomeni na Kabuhoro kwa sh milioni 998.
Akizungumza hii Leo Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (TARURA) Mkoani Mwanza Mhandisi Sobe Makonyo ujenzi huo ulioanza mwezi wa kwanza kupitia Kampuni ya kizalendo ya Nyanza Road Works unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu.
Alisema ujenzi wa barabara hiyo ni kutokana na fedha za serikali huku vilevile eneo hilo zitafungwa taa katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu ili kuwawezesha watu kufanya shughuli zao nyakati za usiku bila ya bughudha yoyote.
“Kwa sasa ujenzi umefika zaidi ya asilimia 60 na tunategemea mradi kutembelewa na mbio za mwenge mwaka huu kwa ajili ya kufungua” alisema Mhandisi Makonyo
Wananchi mbalimbali katika eneo linalopita barabara hiyo wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa jitihada zake kubwa za kuwajengea miundombinu hiyo muda huu wakisema awali ilikuwa ni mibaya ambayo iliwafanya kupata adha nyingi za kusafiri.
Mkaazi wa Mtaa wa Magomeni Gichan Athuman alisema kuwa maendeleo kama hayo walikuwa wakililia muda wote hivyo anashukuru kuanza kwa mradi huo ambao vilevile utawezesha kufungwa kwa taa na kuwepo kwa matuta kuepusha madhara ya ajali.
Alisema vilevile anashukuru utayari wa TARURA kuwasikiliza hivyo kukubali kuwawekea vivuko katika sehemu zilipokuwa zimewekwa kwani hatua hiyo itawawezesha kuvuka bila ya matatizo.
Naye Mhandisi wa Nyanza Road Works Mhandisi Parikshit Sidpara alisema wanashukuru serikali kwa kuendelea kuwaamini katika ujenzi wa barabara mbalimbali hapa mkoani Mwanza na kusema kuwa wao watamaliza mkataba katika muda mwafaka.








