
Kufuatia serikali kuwekeza nguvu kubwa katika kundi la vijana dhidi ya utoaji wa mikopo, Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini Mgore Miraji Kigera amewataka wazazi katika Manispaa ya Musoma kusajili vijana wao wote wanaokaa vijiweni hususani vya pombe ili kuingizwa katika mpango wa mafunzo ya ufundi stadi VETA.
Kauli hiyo anaitoa baada ya baadhi ya wananchi katika mkutano wa hadhara wa usomaji utekelezaji wa siku 100 kulalamikia juu ya uwepo wa vijana katika maeneo ya Majita Road kujiingiza katika vitendo vya ulevi na makundi ambayo yamekuwa yakihatarisha usalama wa wananchi.

Mgore Miraji baada ya malalamiko hayo anawataka wananchi hususani wazazi kuhakikisha wanawashirikisha vijana wao katika mikopo ya serikali lakini pia kutumia ofisi za serikali kupata uelewa juu ya mikopo inayotolewa na serikali ili vijana hao kuingizwa katika mpango na kuondokana na tabia za unywaji wa pombe hovyo.
“Niwaombe wazazi tushirikianeni kuwabaini vijana ili kuwaondoa kwenye makundi hayo, tuko tayari kuwapeleka VETA na kuhakikisha wanaachana na vitendo hivyo, tunahitaji kuijenga Musoma iliyobora na yenye kuhakikisha kila mtu ananufaika na uchumi wa Taifa hili,” Alisema Mgore Miraji Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka alisema serikali imekuwa ikitoa fedha kupitia makundi ya vijana wanawake na watu wenye ulemavu hivyo kamwe hawapaswi kuacha kuchangamkia fursa hiyo.








