
Serikali imesisitiza kuwa uwepo wa anwani za makazi zilizoandaliwa na kutunzwa vizuri ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa kidijitali na uboreshaji wa utoaji wa huduma kwa wananchi. Anwani hizo zinasaidia kutambulisha maeneo ya makazi na kurahisisha huduma mbalimbali za kijamii na kibiashara.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabir Bakari, alisema anwani za makazi ni nyenzo muhimu katika kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kibiashara, ikiwemo posta, usalama, afya, elimu na biashara mtandaoni.

Dk. Bakari aliyasema hayo wakati wa Kongamano la Mwaka la Anwani za Makazi na Maonyesho ya Teknolojia ya Huduma za Posta, akieleza kuwa bila mfumo thabiti wa anwani, jitihada za kujenga uchumi wa kidijitali haziwezi kufanikiwa kwa kiwango kinachotarajiwa.
“Anwani za makazi zinamwezesha mwananchi kutambulika mahali anapoishi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wakati. Ni msingi wa maendeleo ya teknolojia na biashara za kisasa,” alisema Dk. Bakari.
Aliongeza kuwa ni wajibu wa wadau wote kuhakikisha maeneo mapya na yale yanayoboreshwa yanapewa anwani sahihi, ili kuimarisha mifumo ya kidijitali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika la Posta Tanzania, Fredinand Kabyemela, alisema Shirika la Posta linaendelea kuboresha huduma zake kwa kutumia teknolojia, huku akisisitiza kuwa mafanikio hayo yanategemea uwepo wa anwani za makazi zinazotunzwa ipasavyo.
Kabyemela aliongeza kuwa uharibifu au kutojali miundombinu ya anwani husababisha changamoto katika utoaji wa huduma, hivyo kuwakwamisha wananchi na taasisi mbalimbali. “Tunawahamasisha wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya anwani za makazi, kwa kuwa zinagusa moja kwa moja maisha yao ya kila siku,” alisema.








