
Na Boniface Gideon, Tanga
Mbunge wa Jimbo la Tanga, Kassim Amary (Makbel), leo amekabidhi vifaa mbalimbali vya kuwasaidia wanafunzi kujisomea na kujifunzia kwa nadharia na vitendo.
Vifaa hivyo ni pamoja na madaftari, kalamu, vichongeo na vifaa vingine vya kujifunzia.
Akikabidhi msaada huo kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Pongwe yenye mchanganyiko wa wanafunzi wenye ulemavu tofauti, ikiwemo albino, uoni hafifu na ulemavu wa viungo, Makbel alisema msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi zake alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawasimamia watoto katika hatua zote za malezi, ikiwemo masomo, ili kujenga taifa lenye kizazi chenye maadili safi.
“Ndugu wazazi hasa wa jiji letu la Tanga, hakuna sababu ya kumfanya mtoto asiende shule. Ni wajibu wa kila mzazi na mlezi kuhakikisha anamsimamia mtoto ili ahudhurie masomo kila siku. Lakini pia tuhakikishe tunawafundisha watoto wetu maadili mema. Dunia imebadilika sana; hatuwezi kujenga taifa imara kama hatujaweza kusimamia maadili safi,” alisisitiza Makbel.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Pongwe Mchanganyiko, Abubakari Sadik, alimshukuru mbunge huyo kwa kuwapelekea msaada huo wa madaftari ambao umeenda kutatua changamoto ya wanafunzi waliokuwa hawana uwezo wa kununua madaftari kwa wakati.
“Ukosefu wa daftari humfanya mwanafunzi kukosa kumbukumbu za masomo anapofikia kipindi cha mitihani. Hivyo msaada huu umetatua changamoto kwa wengi, kwani wazazi wa baadhi ya watoto wako mbali na inakuwa vigumu kuwa na madaftari kila wakati,” alisema Mwl. Sadik.








