
Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Thecla Mkuchika, ameliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwachukulia hatua watu wote wanaojihusisha na kilimo cha bangi wilayani Butiama mkoani Mara baada ya kukamilisha oparesheni ya kufyeka na kuchoma zao hilo katika kijiji cha Mirwa.

Kauli hiyo ameitoa mara baada ya kukamilisha zoezi la kufyeka na kuteketeza mashamba takribani matatu yaliyokuwa yakilimwa na mwananchi katika eneo la milimani katika kijiji cha Mirwa, ambapo amesema kamwe hakuna atakayebainika kujihusisha na kilimo hicho atakayeponea.
“Kilimo hiki hakiendani na wilaya hii, ni takatifu. Ni aibu kwa wananchi kulima mazao haya. Tunapaswa kumuenzi mwalimu kwa kilimo chenye tija na si kilimo hiki. Niwaombe wananchi wataje wanaofanya vitendo hivyo, tutawachukulia hatua kali,” alisema Bi. Thecla Mkuchika, Mkuu wa Wilaya ya Butiama.

Aidha, alisema kufanya oparesheni za namna hiyo ni kuwasaidia wananchi kujiepusha na kilimo pamoja na matumizi ya zao hilo, huku mmoja wa wananchi waliokutwa katika eneo hilo akiwataka wananchi wenzao kuachana na kilimo cha namna hiyo.








