Home Kitaifa JUDITH KAPINGA ATOA MWELEKEO WA SERIKALI SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA

JUDITH KAPINGA ATOA MWELEKEO WA SERIKALI SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA

Na Magreth Zakaria

Waziri wa Viwanda na Biashara Mh.Judith Kapinga, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha mazingira ya ufanyaji biashara yanakuwa rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa viwanda vya ndani, kukuza bidhaa zinazozalishwa nchini na kupanua masoko ya bidhaa za Tanzania ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 18, 2025 jijini Dar es Salaam, Waziri Kapinga amesema juhudi hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha sekta ya viwanda na biashara nchini ili kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa vijana.

Waziri Kapinga ameainisha kuwa Serikali inaendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya viwanda, ikiwemo upatikanaji wa mitaji, nishati ya uhakika na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uzalishaji.

Ameongeza kuwa hatua zinazochukuliwa zitasaidia kuinua ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na kimataifa, sambamba na kulinda wazalishaji wa ndani dhidi ya ushindani usio wa haki.

Aidha, amesema wizara yake itaendelea kusimamia sera na mikakati itakayowezesha wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kunufaika na fursa zilizopo.

Waziri Kapinga amewahimiza waandishi wa habari kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa sahihi kwa umma kuhusu jitihada zinazofanywa katika sekta ya viwanda na biashara, akisisitiza kuwa mafanikio ya sekta hiyo yanategemea ushirikiano wa wadau wote katika kujenga uchumi imara na shindani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!