Na Shomari Binda-Musoma
JESHI la polisi mkoa wa Mara limewataka wale wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu watafute kazi halali za kufanya kwa kuwa wataishia mikononi mwa polisi.
Kauli hiyo imetolewa na kamanda wa polisi mkoa wa Mara, Salim Morcase, wakati akitoa taarifa za utendaji kazi za jeshi hilo kwa kipindi cha mwezi aprili na mei.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake,Salim amesema hakuna nafasi tena ya wahalifu kufanya uhalifu kwa kuwa wamejipanga kuwadhibiti.
Amesema katika kipindi hicho zaidi ya watuhumiwa 40 wa makosa mbalimbali wakiwemo walio poteza maisha ya waendesha bodaboda tukio lililotokea hivi karibuni wilayani Butiama.
Salim amesema watuhumiwa 11 wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo wamekamatwa na pale uchunguzi utakapokamilika watafikishwa Mahakamani.
Katika oparesheni hiyo amefanikiwa pia kukamatwa mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Daudi Punguja,mkazi wa kwa Mrombo Arusha ambaye alikamatwa na sare pea mbili za jeshi la polisi,kofia 2,mikanda 3 pamoja na pingu vyote vikiwa mali ya jeshi la polisi.
“Nimewaita hapa ndugu zangu Waandishi kutoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi nilichokitaja lakini kubwa niwaambie wale wote wanaojihusisha na uhalifu watafute kazi kazi za kufanya.
“Tumejipanga vizuri kuwashughulikia na vijana wapo na utayari wa kutekeleza jukumu hilo na ndio maana nasema watafute kazi za kufanya”, amesema Salim.
Aidha katika oparesheni hiyo jeshi la polisi mkoa wa Mara limekamata kilogram 416 za madawa ya kulevya aina ya mirungi pamoja na kilogram 6.256 pamoja na miche 19 ya madawa ya kulevya aina ya bangi na watuhumiwa wake 27 wamekamatwa.
Kamanda Salim amewataka wananchi wote wa mkoa wa Mara kuacha mara moja kujihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya.








