Na Theophilida Felician Kagera.
Shirika la KAMEA linalojihusisha na masuala ya huduma ya vyombo vya habari limetoa mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya dhana nzima ya unyanyapaa na ubaguzi kwa watu walioathiriwa na mlipuko wa Ugonjwa wa MARBURG.

Awali akitoa ufafanuzi wa malengo ya kutoa elimu hiyo kwa waandishi wa habari Mkurugenzi wa (Redio Karagwe sauti ya wananchi) inayomilikiwa na shirika hilo Dr Godfry Aligawesa amesema kuwa baada ya Serikali kutangaza kutokuwepo tena kwa ugonjwa huo shirika la KAMEA limeona ni vyema kuungana na wadau wengine kuendelea kutoa elimu kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo ya vyombo vya habari.
“Ni jambo zuri kuisha kwa ugonjwa lakini bado kuendelea kuchukua tahadhari ni muhimu sana, wakati tukiendelea kuhamasisha na kuelimisha jamii kuchukua tahadhari tusiache kutoa elimu hii ya unyanyapaa, mfano kwa wale wenzetu waliokumbwa na maradhi huko Maruku na Kanyangereko unakuta jamii ya maeneo yale inawanyanyapaa kwakuwa na wasiwasi na hofu hali ambayo siyo nzuri ndo maana tumeungana na nyie ili tuweze kusambaza elimu kwa jamii” amesema Mkurugenzi Dr Godfry Aligawesa.
Ameendelea kusema kuwa juhudi zakuwaelimisha wananchi zaidi ili kuwatoa mashaka mashaka ya kuwahisi tofauti waathiriwa zinatakiwa kufanyika kwa kiwango kikubwa jambo ambalo litawasaidia kuelewa vizuri hatimaye isiwepo sababu ya kuwatenga na kuwanyanyapaa.
Ameshauri kuwa elimu hiiyo inapaswa kuenezwa hata kwenye maeneo ya misongamano ikiwemo ya minada ya mifugo hasa ng’ombe , soko na mipakani lengo ni kuhakikisha wananchi na wageni kutoka nje ya nchi wanaelewa kwa upana dhana hiyo.

Mganga Mkuu wa wilaya Karagwe Agnes Mwaifuge akiwa mkufunzi wa mafunzo hayo ametoa pongezi na shukrani kwa wandaaji wa mafunzo pamoja na vyombo vya habari kwa namna vinavyoendelea kutoa habari kwa umma hususani nyakati za milipuko ya magonjwa vimekuwa bega kwa bega nyakati zote za mapambano katika kuwahabarisha mengi wananchi.
Kuhusiana na mada ya unyanyapaa na ubaguzi amesema kuwa juhudi za pomoja zinahitaji kuwaweka sawa wananchi ili kuamini kuwa ugonjwa wa Marburg umekwisha.
“Mgonjwa wa Marburg amepona kwanini tumnyanyapae? kwahiyo haina haja kufanya hivyo hata angekuwa bado anamaambukizi tunatakiwa tumtie moyo kuwabagua hawa hatutawasaidia katika maana kwamba tukiwabagua na kuwanyanyapaa itatokea shida nyingine hawatatoa taarifa badala yake watajifugia ndani” Mganga Mkuu Mwaifuge akitoa soma kwa waandishi wa habari.
Ameeleza kwamba dhana ya unyanyapaa ni mbaya kwani huleta madhara mbalimbali kwa mtu aliyekumbwa na jambo lolote yakiwemo magonjwa hatarishi kama vilel MARBUG, COVID 19, HIV na mengineyo wakati mwingine huitwa majina mabaya ambayo huwapelekea kuishi kwa hofu na kukata tamaa kabisa hatimeya kuchukua maamzi ambayo siyo sahihi kwao maana hata vifo huweza kujitokeza kutoka na hali hiyo.
Amewahimiza na kuwasihi wa waandishi wa habari Mkoani Kagera kuendelea kutoa elimu na kuwapa taarifa sahihi wananchi ili kuwasaidia kuwaondoa hofu na wasiwasi kwa jambo lolote lenye kuwanyima amani yakiwemo magonjwa.
Waandishi wa habari wa vyombo vya habari ambavyo ni Redio, TV Magazeti na Oneline kutoka wilaya ya Karagwe na nje ya Karagwe wamenufaika na mafunzo hayo ambayo yamewajengea uwezo wakuendelea kufanya kazi zao kwa ufanisi hasahasa katika kuandika habari zinazohusiana na milipuko ya magonjwa.








