
Na Abdala Sifi WMJJWM – Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuongeza bidii na kasi zaidi katika kutimiza wajibu wao ili kuharakisha maendeleo ya jamii.
Dkt. Gwajima amesema hayo leo Novemba 17, 2025, alipowasili katika Ofisi za Wizara hiyo baada ya hafla ya kuapishwa kuendelea kuongoza Wizara hiyo kwa kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Sita.

Dkt. Gwajima amesema kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Sita kilitumika kuijenga Wizara mpya kwa kuanzisha mifumo ya uendeshaji, uwajibikaji, kutunga sera mbalimbali, mikakati, miongozo ya kisera na programu kadhaa za utekelezaji sambamba na kuitambulisha Wizara kwa jamii na wadau wa maendeleo.
Ameongeza kuwa kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Sita kitajikita katika kujenga ushirikiano na mshikamano wa wadau wote katika kuelimisha jamii kuhusu uwepo wa fursa mbalimbali za kiuchumi na kuwasaidia kuzifikia, kwani umaskini unachangia sehemu kubwa ya ukatili wa kijinsia na kwa makundi maalum.
“Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuniamini na kuniteua tena kuongoza Wizara hii, na imani hii na heshima hii ni yenu pia kwa kuwa mlinipa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yangu, hivyo basi nawaomba tena tuendelee kufanya kazi kwa spidi zaidi, ari na ufanisi ili kutimiza azma ya Serikali,” amesema Dkt. Gwajima.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Maryprisca Mahundi, amewashukuru watumishi wa Wizara kwa mapokezi na kusema yupo tayari kufanya kazi, hivyo ameomba ushirikiano ili kufanikisha malengo ya Wizara na Serikali.
Awali, akiwakaribisha viongozi hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amewapongeza kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, na kuwaahidi kupata ushirikiano kutoka kwa Menejimenti na watumishi wa Wizara hiyo.








