
Balozi zimeombwa kuwarejesha nchini wachochezi wa vurugu za tarehe 29 Oktoba wanaoishi nje ya Tanzania, hususan Kenya na Marekani, ili wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.
Hayo yamesemwa leo Disemba 17, 2025 na mwenyekiti wa Media Center for Information and Resources Advocacy (MECIRA), Habibu Mchange, wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa watu hao wanahusika moja kwa moja na kuchochea machafuko, mauaji na kudharau mamlaka ya nchi.
Mchange amesema wahusika wanatambulika walipo, na kusisitiza kuwa lazima warejeshwe nchini ili kujibu kesi zinazowakabili, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda amani ya taifa.
Ameeleza kuwa wachochezi wa vurugu wanawajibika moja kwa moja kwa madhara yaliyotokea ikiwemo vifo, akisisitiza kuwa hakuna haki bila wajibu kwa yeyote aliyeshiriki kupanga au kuchochea machafuko.
Aidha, amesema Maria Sarungi alikimbilia Nairobi kisha Skandinavia, na kwamba hatua zinaendelea kuchukuliwa kumfuatilia na kumfikisha katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) pamoja na wachochezi wengine ili wakamatwe na kuwajibishwa kisheria.








