Na Shomari Binda-Musoma
WAZIRI wa mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Yusuf Masauni amezindua zoezi la kitaifa la ugawaji vitambulisho vya taifa mkoani Mara.
Akizungumza kwenye zoezi la uzinfuzi huo kwenye uwanja wa shule ya msingi Mukendo mjini Musoma amesema uzinduzi huo ni tamati ya tatizo la upatikanaji wa vitambulisho.
Amesema vitambulisho vina umuhimu mkubwa katika kuwasaidia wananchi kwenye kupata huduma mbalimbali za kijamii.
Waziri Maaauni amesema Mamlaka ya Vitambulisho vya TAIFA ( NIDA) imeongeza kasi ya kuzalisha na kusambaza vitambulisho vikiwa ni vyenye ubora.
Amesema zoezi hilo wameamua kulianzia mikoa ya pembezoni na baadae litaendelea nchi nzima katika kugawa vitambulisho hivyo.
“Baada ya uzinduzi huu hapa uwanjani zoezi hili litaendelea kwenye vitongoji,vijiji na mitaa yetu hivyo nitumie nafasi hii kuwaomba viongozi kwenye maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa maafisa wa NIDA”
“Zoezi hili lisichukuliwe kama la NIDA peke yao bali ni la kila mmoja wetu na tumejipanga ifikapo mwezi desemba kila mwananchi aliyesajiliwa anapata kitambulisho chake” amesema Waziri Masauni.

Mkuu wa mkoa wa Mara Saidi Mtanda amesema maafisa wa NIDA wanapaswa kugawa vitambulisho hivyo pasipo vikwazo vyovyote kwa wananchi.
Amesema mwananchi yoyote atakayekutana na vikwazo ikiwemo kuombwa pesa ili apate kitambulisho atoe taarifa kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya aliyopo au ofisi ya mkuu wa mkoa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa vitambulisho vya Taifa( NIDA) Mhandisi Ismail Rumatila amesema watu zaidi ya milioni 24 wamesajiliwa na wanatarajiwa kupata vitambulisho vyao.









