
Na Magrethy Katengu— Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA, ametoa maelekezo kwa viongozi na wadau wa sekta ya vitabu nchini, akitaka hatua za haraka zichukuliwe kuimarisha uchapishaji, uandishi, usomaji na ulinzi wa haki miliki za waandishi.
Mwinjuma ametoa maelekezo hayo leo, Oktoba 12, 2026,Jijini Dar es salaam wakati akifungua rasmi Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Vitabu Tanzania, yaliyofunguliwa kwa shughuli zake Oktoba 10, mwaka huu.

Amesema vitabu vina nafasi muhimu katika kuhifadhi historia ya taifa, kuendeleza lugha ya Kiswahili, kukuza maarifa na kulinda utamaduni, hivyo kuna umuhimu wa kuweka mazingira bora yatakayowezesha waandishi na wachapishaji kufanya kazi zao kwa ufanisi.
“Naelekeza Wizara pamoja na taasisi zake kuitisha kikao kazi kitakachowakutanisha wadau wa sekta ya vitabu na uandishi ndani ya wiki mbili zijazo, kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya utekelezaji wa hoja zilizowasilishwa na Chama cha Wachapishaji wa Vitabu Tanzania (PATA)”amesema Naibu Waziri
Aidha, amewaagiza watendaji wa Wizara na taasisi zake kuwasilisha taarifa ifikapo Ijumaa, Oktoba 16, 2026, zikieleza hatua zilizochukuliwa kutekeleza maelekezo yaliyotolewa awali na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi.
Katika hatua nyingine, Mwinjuma ameitaka Bodi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA), kwa kushirikiana na PATA, kuwasilisha taarifa kuhusu operesheni zilizofanyika na kesi zinazohusu uharamia wa kazi za waandishi, ili kuweka wazi hatua zinazochukuliwa kukabiliana na vitendo vinavyokiuka haki zao.
Naunga mkono mapendekezo yaliyotolewa na PATA, yakiwemo kuanzishwa kwa jukwaa la kuwatambua waandishi mahiri litakalojulikana kama Swahili Hall of Fame, kufufua tuzo za Shaaban Robert na Zeze, pamoja na kuanzisha Maktaba ya Kimataifa ya Kiswahili
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) inayoisimamia Maktaba Kuu ya Taifa ni Dkt. Mboni A. Ruzegea. amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, bodi hiyo imejipanga kununua nakala 100,000 za vitabu kutoka kwa wachapishaji wa ndani, hatua inayolenga kuwawezesha wachapishaji kukuza biashara zao na kuongeza upatikanaji wa vitabu nchini.
Amesema bodi hiyo pia inalenga kuwafikia watumiaji zaidi ya 800,000 kote nchini kupitia huduma zake za maktaba.
Amesema bodi hiyo pia inalenga kuwafikia watumiaji zaidi ya 800,000 kote nchini kupitia huduma zake za maktaba.
Amesisitiza kuwa usomaji ni msingi wa maarifa na maendeleo ya jamii katika ulimwengu wa sasa unaoendelea kutegemea teknolojia, akionya kuwa matumizi ya teknolojia bila msingi wa maarifa yanaweza kuleta changamoto katika maendeleo ya mtu binafsi na taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa PATA, Hemedi Damian, amesema maonesho hayo yamewakutanisha wadau na taasisi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, zikiwemo taasisi za utamaduni kutoka Iran na Urusi, Ofisi ya Bunge la Tanzania na Uongozi Institute.
Amesema maonesho hayo ni fursa muhimu ya kukuza sekta ya vitabu, kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wadau na kuwapa wananchi nafasi ya kupata vitabu vinavyoongeza maarifa na kuhamasisha utamaduni wa kusoma.
Yameandaliwa na Chama cha Wachapishaji wa Vitabu Tanzania PATA, yakitoa fursa kwa Watanzania, wanafunzi, shule na taasisi mbalimbali kujionea kazi za waandishi, ubunifu na vipaji vilivyopo katika sekta ya uandishi na uchapishaji nchini.
Kupitia maonesho hayo, washiriki wanapata nafasi ya kutambua mchango wa vitabu katika kukuza maarifa, kuimarisha elimu na kuhifadhi utamaduni, huku yakitoa jukwaa la kukutana na kubadilishana uzoefu kati ya waandishi, wachapishaji na wasomaji.
Aidha, maonesho hayo yamehusisha kazi kutoka kwa wadau wa ndani na wa kimataifa, zikiwemo taasisi na nchi za nje kama Iran na Urusi, hali inayotoa fursa ya kujifunza tamaduni, maarifa na mitazamo mbalimbali kupitia maandishi.
Maonesho ya Kimataifa ya Vitabu Tanzania ni sehemu ya juhudi za kukuza sekta ya vitabu nchini na kuwahamasisha wananchi, hususan watoto na vijana, kujenga utamaduni wa kusoma na kutumia maarifa yanayopatikana kupitia vitabu kwa maendeleo binafsi na ya taifa.









