Home Kitaifa DKT. SEIF ASISITIZA KUKAMILIKA KWA MIRADI YA AFYA MWANZA

DKT. SEIF ASISITIZA KUKAMILIKA KWA MIRADI YA AFYA MWANZA

Watendaji wote waliopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wameelekezwa kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa miradi ya maendeleo, wakisisitizwa umuhimu wa miradi hiyo kukamilika kwa wakati ili kuleta manufaa kwa walengwa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Jafar Seif, wakati wa ziara yake mkoani Mwanza alipokutana na viongozi wanaosimamia Sekta ya Afya na kukagua ujenzi wa jengo la ghorofa tano la Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana. Ujenzi wa jengo hilo umefikia hatua ya ngazi ya sakafu ya kwanza (slab) na unatarajiwa kukamilika mapema Januari 2026.

Aidha, Dkt. Seif amesisitiza kuwa thamani ya fedha inayotolewa na Serikali inapaswa kuonekana wazi, huku viongozi wa Serikali wakitakiwa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Adv. Kiomoni Kibamba, amesema mradi huo ulitazamiwa kukamilika baada ya kipindi cha miaka nane kutokana na changamoto za kibajeti, na kukamilika kwake kutaongeza uwezo wa utoaji wa huduma za dharura pamoja na kupunguza rufaa zinazokwenda Hospitali ya Mkoa na Kanda.

Katika ziara hiyo, Dkt. Seif pia ametembelea Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, Kituo cha Afya Buswelu na kukagua Zahanati ya Nyambiti iliyokamilika, ambapo kuanza kwa utoaji wa huduma kwa jamii kunatarajiwa kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Kituo cha Afya Buzuruga wilayani Ilemela.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!