
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amewataka watendaji wa Wizara ya Afya kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu, na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuleta tija na ufanisi kwa wananchi.
Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo leo, Novemba 18, 2025, alipokutana na Menejimenti ya Wizara mara baada ya kuwasili rasmi kuanza majukumu yake mapya ya kazi katika Wizara hiyo.

Amesema huu ni wakati wa watumishi kuongeza juhudi na kutojibweteka ili kuendelea kusukuma maendeleo ya Sekta ya Afya mbele.
“Nawasisitiza watumishi wote kuacha kufanya kazi kwa mazoea. Tubadilike na kutekeleza majukumu kwa ufanisi ili kuhakikisha Taifa letu linasonga mbele katika Sekta ya Afya,” amesema Mhe. Mchengerwa.
Aidha, Waziri Mchengerwa amewataka watumishi wote kufuata maadili ya kazi na kusimamia kwa umakini maelekezo yanayotolewa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.









