
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ameshiriki Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC–Organ Troika Summit) kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika kwa njia ya mtandao akiwa Babati, mkoani Manyara.

Mkutano huo umeongozwa na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Malawi, Mhe. Prof. Arthur Peter Mutharika.
Viongozi hao wamejadili hali ya kisiasa na usalama katika Jamhuri ya Madagascar kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika hivi karibuni. Aidha, mkutano umeweka dhamira ya kuunga mkono juhudi za kurejesha hali ya amani na utulivu nchini humo, pamoja na kutoa wito kwa wananchi wa Madagascar kutumia njia ya mazungumzo katika kukabiliana na hali iliyopo, na kuachana na vurugu, uporaji na uharibifu wa mali.
Kadhalika, mkutano umeiagiza Sekretarieti ya SADC kuhakikisha inashirikisha wadau muhimu kama vile Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Nchi za Bahari ya Hindi, ili kuwe na uratibu wa pamoja katika kutafuta suluhu ya mgogoro nchini Madagascar.